Latest Updates

KANUNI 6 ZA KUACHANA NA MPENZI WAKO AMBAYE UNAHISI UMEMCHOKA KWA SABABU MOJA AU NYINGINE





Uchunguzi unaonesha kuwa, wanawake/wanaume wengi husumbuka sana kutafuta njia za kukatisha uhusiano wao wa kimapenzi na wapenzi wao baada ya kugundua kuwa hawako kwenye chaguo sahihi kwa sababu moja au nyingine....

Wengi wao hujikuta wanashindwa kufikia lengo hilo kwa sababu ya kutoeleweka na wapenzi wao. Dondoo za mahojiano zilizofanyika kwa  baadhi ya wanawake zinaonesha kuwa, asilimia 48 kati yao wanaishi kwenye mapenzi ya lazima au yaliyowachosha.

Utakuta  wanawake wengi wanasema maneno kama haya hapa chini.....
“Sina la kufanya, nimemwambia mara nyingi tuachane lakini hasikii, ananitisha kuwa nikimwacha atanikomesha. Anachofikiri nimepata mwanaume mwingine lakini ukweli tabia zake zimenichosha,” 

Kisaikolojia mapenzi ya kulazimisha nafsi yamekuwa na madhara makubwa kiafya na kiufahamu. Wengi kati ya watu waliotokea kuua, kujiua au kujeruhi wanatoka katika kundi la maisha ya mapenzi ya lazima. 
 
Chukua hatua zifuatazo kama umeamua kuachana na mpenzi wako uliyemchoka.

1. KUWA MKWELI
Wanawake/wanaume wengi wamekuwa wakificha sababu za kutaka kuachana na wapenzi wao wakihofia kuwaumiza au kujiumbua. Ukweli unamtaka mwanamke amwambie wazi mwanaume kwa nini anataka kukatisha uhusiano.  Mweleze ajue kasoro zake na uweke wazi hali ya kuchoka kumvumilia kuwa nae.

2. MUDA SAHIHI
Usikurupuke kuachana na mpenzi wako. Lazima uhakikishe kuwa uko kwenye wakati sahihi ambao hautakufanya ujutie uamuzi wako. Ikiwa unajua kuna gari umemuazima, pesa, mali na vitu vingine vya thamani tafuta njia za kuzuia visipotee. Ushauri wa kitaalamu kuhusu mali ni muhimu ukauzingatia kabla ya kuamua.

3. SHIRIKISHA WATU
Ukiwa umehakiki mawazo yako usimwambie mhusika mkiwa chumbani. Weka wazi azimio lako mbele ya rafiki na ndugu. Faida za kufanya hivi ni kuweka ushahidi na wakati huo huo kumharibu kisaikolojia asiweze kurudi kwako kwani wanaume wanatajwa kuwa na aibu ya kuonekana wanang’ang’aniza penzi.

4. FANYA MWENYEWE
Suala la kuachana ni binafsi, hivyo unapofikia hatua hiyo lazima uwe ni wewe uliyeamua kufanya hivyo na isiwe shinikizo kutoka kwa watu wengine kwa masilahi yao. Kama "ulivyopenda" ndivyo "uache".

5. UMAANISHE 
Kuna wanawake/wanaume ambao hutangaza kuwaacha wapenzi wao, lakini hawamaanishi sawa na uamuzi wao. Utakuta pamoja na hatua hiyo huendelea kuwatumia meseji za mapenzi, kujichekesha chekesha, kujipitisha pitisha na wakati mwingine hata kujipeleka nyumbani. Kufanya hivyo hakuwezi kuleta matokeo sahihi.

6. USIRUDI NYUMA
Uamuzi wa kuachana lazima uwe umeshiba sababu ili isijitokeze hali ya kurudi nyuma na kujuta. Mwanaume ukishamtangazia kumwacha, halafu akaona unajirudisha mwenyewe utamfanya aamini kuwa huna pa kwenda na hivyo kama alikuwa anakutesa na kukudharau ataongeza zaidi. Utakuwa uni kama unasukuma ukuta wakati upo ndani ya nyumba.

Hizi ni baadhi ya kanuni kati ya nyingi ambazo unaweza kuzichukua ili kuachana vizuri na mpenzi wako ambaye unahisi umemchoka kwa sababu moja au nyingine......

0 Response to "KANUNI 6 ZA KUACHANA NA MPENZI WAKO AMBAYE UNAHISI UMEMCHOKA KWA SABABU MOJA AU NYINGINE"

Post a Comment