Latest Updates

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO

MARAFIKI na mpenzi wako ni nani bora? Kabla hujajibu fumba kwanza macho kisha tafakari. Umeshapata jibu? Usijibu, hebu vuta picha kwa mara ya pili, fanya tafakuri ya kina kisha lipime jawabu lako. Kile ambacho umepata ndiyo muongozo wa kila siku katika maisha yako.
Hata hivyo, naomba nikupe changamoto kupitia hilo jibu lako. Kuna kipindi marafiki wanaweza kuwa muhimu kuliko mwenzi wako, vilevile zipo nyakati zikifika, haitawezekana kumpa rafiki kipaumbele kuliko mpenzi wako. Hapa inataka maarifa na akili tulivu kuchanganua.
Rafiki anaweza kuwa muhimu kipindi unamsoma mwenzi wako. Hata hivyo, umuhimu wake una ukomo, kwani hatakiwi kuchukua akili yako au kumpa hata asilimia 50 ya mawazo juu ya kile ambacho unataka kukiamua. Asilimia 15 zinamtosha, kisha zingatia; akili za kuambiwa changanya na zako.
Maisha yako yapo ndani yako mwenyewe. Unachohitaji au kukitamani katika maisha yako ya kimapenzi, unakijua wewe. Kama ndivyo, basi tambua kuwa ukimsikiliza sana rafiki, anaweza kukupotosha. Matokeo yake anaweza kukufanya uishi ndani ya matarajio yake.
Wewe na yeye, kila mmoja ana sifa zake anazoziangalia kwenye mapenzi. Una sifa ambazo unadhani mwenzi wako akiwa nazo maisha yako yatakuwa na furaha, naye anavyo vipengele ambavyo anataraji ‘waubavu’ wake awe navyo ili amani na upendo vitawale.
Mathalan, unaamini kuwa mwenzi wako anapaswa kuwa mtanashati, mzuri wa umbo na sura lakini mwenzako anaamini kwamba vyote hivyo ni sawa lakini kama tabia yake siyo nzuri hafai. Hapo utakuwa umeshaona namna ambavyo wewe na yeye mnatofautiana. 
Unaamini katika mpenzi mwenye mapenzi ya kweli, anayejali, mwelewa, asiye na gubu, mwaminifu, rafiki yako kipaumbele chake ni kumpata mwenye fedha. Hapo ikupe picha kuwa wewe ni wewe na yeye ni yeye. Ukizubaa, utapoteza matarajio yako kwa sababu ya kushikiwa kichwa na rafiki yako.
Ni dhambi kubwa, tena ni usaliti wa hali ya juu kuacha misingi ambayo wewe unaamini inaweza kukupa furaha, utulivu na amani ya moyo na kufuata ushauri wa rafiki yako ambaye hana uwezo wa kusoma hisia zako na kujua nini hasa unahitaji. Atadhani upo kama yeye, kwa hiyo atakwambia ufuate anachopenda yeye.
Ipo mifano ya watu wanaoteseka leo kwa sababu ya kupotoshwa na marafiki. Walikuwa na wapenzi wazuri sana, waliokuwa wanasikilizana nao lakini wakaachana baada ya kushauriwa ndivyo sivyo. Picha iliyo wazi kwa sasa, mapenzi kuwa na vurugu nyingi, ikufanye uelewe mantiki ya hoja ambayo naijenga.
Kama marafiki wenyewe wanachukuliana wapenzi, ni kwa nini isikupe sababu ya kuamini kwamba wewe upo sahihi zaidi kwenye uamuzi wako kuliko mshauri? Pengine akakujaza maneno ya chuki kwa mwenzi wako, mwisho ukamwona hafai, baada ya majuma mawili unagundua yupo naye.
Ukiweka pembeni hoja ya kuchukuliana wapenzi, ukweli mwingine ni kwamba rafiki anaweza kukufanya uachane na mwenzi wako mnayependana na kuelewana vizuri ili ukajiweke kwa mwenye fedha. Mwisho wa hilo siku zote kuna majuto, kwa maana pesa itakuwezesha kutatua mambo mengi lakini haziwezi kukupa penzi linalokidhi moyo.
Kama ambavyo umewahi kushuhudia mateso ya mtu kulazimishwa kuoa au kuolewa na yule asiyempenda kwa sababu mbalimbali, hususan kichocheo cha shinikizo la wazazi, ndivyo hutokea pale uhusiano unapojengwa na fedha. Shika neno hili kuwa binadamu ni rahisi sana kuzizoea fedha pale anapokuwa anazipata.
Anapozoea maisha ya fedha, moja kwa moja humuona wa kawaida sana, yule mwenzi wake aliyemkubali kwa sababu ya mali. Ni hapo ndipo humsaka yule atakayempa tulizo la kweli la moyo. Vitendo vya wenye fedha wengi kusalitiwa, ikupe sababu ya kuyazingatia haya.
Kwa nini baadaye uje kuvuna aibu ya kuonekana msaliti? Amua leo kwamba pamoja na hali yoyote ya kimaisha uliyonayo na mwenzi wako, mtalindana kwa shida na raha. Yote yanawezekana, endapo kwa maelewano yenu na nia ya dhati, mtajitolea kusaka maisha bora zaidi, yatapatikana tu.

0 Response to "MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO"

Post a Comment