Latest Updates

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-3


Tunaendelea na mada yetu tuliyoianza siku kadhaa zilizopita. Tunaendelea kuanzia pale tulipokuwa tumeishia.
Upande wa pili, kuna ulimi wako. Kipi ambacho unakitamka kuzungumza na watu? Ni nini unachomwambia mwenzi wako? Kwa pamoja, vitu hivyo, vinaweza kuufanya uhusiano kuanguka kutoka kwenye uimara wake hadi kuwa legelege kabla ya kuvunjika kabisa.



Kasoro kubwa ambayo watu wengi wanayo ni kutochunga ndimi zao siku za mwanzo za kukutana na wapenzi wao. Aghalabu, mtu anakuwa anahisi huyo aliye karibu naye ni wa kupita tu, kwa hiyo anaamua kuzungumza vitu ambavyo baadaye humletea shida. Tena shida kwelikweli!
Nashauri kila mtu awe na nidhamu ya kuzungumza pale anapokuwa na mtu ambaye kuna dalili ya kuingia naye kwenye uhusiano wa kimapenzi. Huwezi kujua utasafiri naye mpaka wapi, kwani wengi wameoana lakini ndoa zao zinaishi kwa staili ya kusutana kila leo, wakikumbushana maneno waliyoambiana nyakati zilizopita.

ZINGATIO LA KISAIKOLOJIA
Nyakati za mwanzo za uhusiano wa kimapenzi, watu wengi huficha kucha. Unaweza kumwambia mwenzio kitu ambacho kinaweza kumfanya aone kinyaa hata kuendelea na wewe lakini asikasirike. Pengine akakuunga mkono au akakushauri kwa lugha iliyotulia.
Hata hivyo, jambo hilo unalomwambia halitakwisha kichwani kwake. Pale atakapokuwa amekuzoea, ataanza kukushusha thamani kila anapokumbuka yale matamshi yako. Juu ya yote hayo, matokeo yake ni kuvunjiana heshima kwa kukumbushana mambo ya kuumiza.
Huumiza kwa sababu pale mwanzoni alipokuwa anazungumza hakuwa na mapenzi ya dhati kama anayoweza kuwa nayo baadaye mapenzi yanapomkolea.
Sasa basi, dawa ni kuchunga ulimi wako ili baadaye usije ukajuta pale utakapokuwa unakumbushwa. Nenda salama, tena tembea juu ya karatasi nyeupe, baadaye utajionea mwenyewe jinsi ambavyo maisha yako ya kimapenzi yanaweza kuwa rahisi na matamu kuliko kawaida.
MFANO; Jane alipokuwa anaanza uhusiano wa kimapenzi na Raja, alidhani mapenzi yao ni urafiki na yatapita tu. Hivyo basi, mwanzoni Jane akawa anaweza kutamka maneno magumu, akiwaambia rafiki zake, huku Raja akisikia. Hakumhofia kabisa kwa lolote.
Siku moja, rafiki yake alimtania, akamwambia: “Usisahau kutumia kondomu, utapata mimba isiyotarajiwa.”
Jane akajibu: “Nikipata mimba ‘naflash’, mbona kitu rahisi?”
Yule rafiki wa Jane akaongeza: “Umezoea eeh, shauri yako?”
Raja ambaye alikuwa anasikiliza yale mazungumzo, alikasirishwa sana na utani ule. Kuanzia pale yule rafiki wa Jane alipoanzisha, maana aliona anamkosea heshima, pili namna ambavyo Jane alijibu, alishangaa sana. Hata hivyo, Raja hakutia neno, alivumilia kwa sababu mapenzi ndiyo kwanza yalikuwa yanaanza.
Siku zilivyokwenda mbele, Raja alimzoea Jane. Sasa akawa na ujasiri wa kuhoji baadhi ya vitu. Siku moja Raja aliumwa na kulazwa kwenye hospitali moja iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam. Jane alipokwenda kumwona, akamwambia: “Baby hii hospitali wanatoa sana mimba.”
Raja akashtuka kuisikia kauli hiyo kutoka kwa mwenzi wake, akaiunganisha na ya siku ile alipokuwa anataniana na rafiki yake: “Nikipata mimba ‘naflash’, mbona kitu rahisi.” Vilevile, Raja akayakumbuka maneno ya yule rafiki wa Jane: “Umezoea eeh, shauri yako!”
Hapohapo, Raja akamuuliza Jane: “Wewe umejuaje kama hapa wanatoa mimba?”
Jane akajibu: “Najua tu, si unajua mimi ni mwanamke?”
Raja: “Ukiwa mwanamke ndiyo ujue sehemu za kutoa mimba?”
Jane: “Je, nikisema nimeshatoa mimba hapa?”
Raja: “Hapo unamaanisha wewe ni mzoefu wa kuchoropoa mimba siyo?”
Jane: “Una maanisha nini kuniita mzoefu?”
Raja: “Kauli zako zinatoa picha. Siku ile ulisema ukipata mimba unaflash, leo umefika hapa hata hatujaongea kuhusu ugonjwa wangu, wewe unasema hapa wanatoa mimba. Asimuliaye mvua imemnyeshea.”
Jane: “Labda kama una yako, nisikwambie kitu ninachokijua? Wewe siku hizi una wivu sana.”
Raja: “Jane naanza kupata picha mbaya sana kwako. Huko nyuma ulishanitamkia kuwa wewe unapenda sana ngono, tena ulikuwa mzinzi sana. Na hili la utoaji mimba. Maneno yako yanaonesha wewe ni mwanamke malaya sana.”

0 Response to "MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-3"

Post a Comment