Latest Updates

MAWASILIANO FINYU NI ISHARA KUWA HUPENDWI, USING’ANG’ANIE!

MAWASILIANO FINYU NI ISHARA KUWA HUPENDWI, USING’ANG’ANIE!
HIVI kwa nini mapenzi yanatuweka katika wakati mgumu kiasi hiki? Watu wanalia kila siku sababu ikiwa ni kupenda pasipo na penzi. Uvumilivu unakuwepo mtu akiamini huenda mambo yatabadilika lakini matokeo yake hali inazidi kuwa mbaya.
Hapo ndipo utamkuta mtu akiwa njia panda. Anampenda mtu lakini hapati kile alichotarajia. Amemzimikia mtu weee lakini anashangaa mawasiliano yanakatika ghafla, akiuliza anaambulia jibu la ‘niko bize, nitakutafuta’.
Naomba leo nizungumzie hili la mawasiliano finyu kwa wapenzi na jinsi ambavyo linachukuliwa kama ishara ya kutokuwepo kwa penzi la dhati.
Katika mazingira ya kawaida, penzi linajengwa na mihimili mingi na mojawapo ni mawasiliano. Wanaopendana kwa dhati, watapenda kila wakati wawe pamoja na kama kutakuwa na mazingira ya wao kuwa mbalimbali, simu zitatumika kuwafanya wajihisi wako pamoja.
Ndiyo maana tunaambiwa, itumie simu yako kumfanya mpenzi wako ahisi uko karibu naye. Kama uko mbali naye, asubuhi unatakiwa kumsabahi kwa maneno matamu, mchana ukifika vivyohivyo na usiku wakati wa kulala ndipo wengi hutumia nafasi hiyo kulipaka rangi penzi lao.
Utakuwa ni mtu wa ajabu sana kama utapitisha siku nzima bila kuwasiliana na mpenzi wako kwa kigezo kwamba eti uko bize. Jamani, tunajua kazi ni muhimu sana katika maisha ya binadamu lakini ubize isiwe sababu ya mpenzi wako kuhisi haupo naye.
Wiki inapita, eti ndiyo unamtafuta mpenzi wako halafu ukiulizwa unadai ulikuwa bize na kazi. Mpenzi wako anakutumia sms nzuri lakini wewe hujibu au kama ukijibu inakuwa kwa kifupi sana, kisingizio kikiwa ni kazi.
Mpenzi wako anakupigia, hupokei. Yaani unachukulia kama usumbufu vile. Au yeye kila siku anakuwa wa kwanza kukupigia, wewe wala huna taimu. Kwa kweli katika mazingira hayo, penzi la dhati linakuwa halipo na kama mpenzi wako anakufanyia hivyo, ujue huna mtu. Anza kuangalia ustaarabu mwingine.
Wataalamu wa mambo ya mapenzi wanasema kuwa, ukiona mpenzi wako anapunguza mawasiliano ujue hiyo ni hatua ya kukuchoka. Haoni umuhimu wa kuwasiliana na wewe kama zamani na kama akifanya hivyo, ujue ana shida yake.
Inawezekana alishakuzoesha kukupigia simu kila wakati au kukutumia sms za kukujulia hali, lakini sasa hafanyi hivyo. Ukiona alama hii ujue mwisho wa penzi lenu unakaribia.
Haishangazi sana kuacha kukupigia simu kwa wiki nzima, lakini siku atakayokupigia utakutana na maneno haya; “Nina hamu sana na wewe mpenzi wangu, njoo basi leo ulale nyumbani kwangu, naamini hutaniangusha!” Hapa anahitaji penzi lako ndiyo maana anakuambia kwa sauti laini kama hii na baada ya kupata anachohitaji, anakuweka ‘pending’.
Mbali na hilo la mawasiliano, pia ukiona mpenzi wako anakuwa mgumu kukutana na wewe jua penzi linaelekea ukingoni. Unaweza kuona ghafla anakuwa mtu wa mambo mengi, kumpata kwake siyo rahisi.
Anajifanya mtu wa kazi nyingi ambazo mwanzoni wakati mnakutana hakuwa nazo! Kipindi hiki anakuwa na visingizio vingi visivyokuwa na maana lakini lililokuwa akilini mwake ni kukwepa kuonana na wewe.